Description
Dalili Za Unabii
Dalili Za Unabii([1])
Hakika sifa njema zote ni za Allah, twamsifu yeye na kumtaka msaada wake na msamaha wake, na tunajilinda kwa Allah kutokana na shari za nafsi zetu na maovu ya vitendo vyetu, atakayeongozwa na Allah basi hakuna atakayempoteza, na atakayempoteza basi hakuna atakayeweza kumuongoza, na nashuhudia ya kwamba hapana apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah peke yake pasina mshirika, na nashuhudia ya kwamba kwa hakika Muhammad ni mja na Mtume wa Allah, rehema za Allah na amani ziwe juu yake na familia yake na maswahaba wake
Baada ya hayo:
Mcheni Allah- enyi waja wa Allah- hakika ya kumcha, na mchungeni katika siri na minong'ono
Enyi waislamu:
Kwa hakika Allah amewatuma mitume ili kuwaongoza viumbe, wanakamilisha umbile (fitra([2])) kwa nuru ya wahyi walioteremshiwa, na wanawalingania watu kwenye ibada za Allah, matendo mema, tabia njema, na wanadamu wanawahitajia mitume zaidi kuliko vile wanavyohitajia chakula na kinywaji na pumzi; kwani hakuna njia kamwe ya kupata furaha, kufaulu na kupata radhi za Allah isipokuwa kupitia mikono yao.
Na Allah mtukufu amepwekeka kwa ukwasi kamili, na uwezo mkamilifu, na elimu inayozunguka kila kitu, nao mitume ni wanadamu wala hawamiliki chochote katika mambo haya matatu ila waliyopatiwa na Allah, Amesema Allah aliyetukuka kumwambia Mtume wakeﷺ : ﴾"Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina hawa, "Mimi sidai kuwa ninamiliki hazina za mbingu na ardhi nikawa nazitumia nitakavyo; na sidai kuwa mimi najua al-ghayb (yasiyoonekana); na wala sidai kuwa mimi ni malaika"﴿, Allah amewahusu kutokana na uwezo wake na elimu yake na ufalme wake kwa alama na miujiza yenye kuvutia; Ili iwabainikie waja kuwa wao ni mitume wa Allah walio wakweli katika yale waliyotolea habari, Amesema Mtume ﷺ: «Hakuna nabii yeyote katika manabii isipokuwa alipewa miujiza iliyokuwa sababu ya kuaminiwa na wanadamu» imepokewa na Bukhari na Muslim
Alikuja Nabii Swãlih -amani iwe juu yake- na ngamia mkubwa aliyetoka kwenye jiwe.
Naye Nabii Ibrãhim -amani imshukie- alitupwa kwenye moto mkubwa; wala haukumuudhi.
Na Nabii Mûsã - amani imshukie- alipewa aya tisa zilizokuwa wazi, akaipiga bahari kwa fimbo, nayo bahari ikapasuka, kila kipande mfano wa jabali kubwa, na akatupa chini fimbo yake ikawa joka kubwa.
Nao Nabii Dāwūd na Sulaymān -amani iwashukie-walifahamishwa mantwiqa attwair yani lugha na maneno ya ndege na wakapewa kila kitu kinachohitajika.
Naye 'Ĩsã amani iwe juu yake alikuwa akiwaponya waliozaliwa vipofu na wenye barasi na kuwahuisha wafu kwa idhini ya Allah, na akawaongelesha watu akiwa mtoto mchanga wa kunyonya kabla ya kufikia wakati wa kusema, akamtakasa mamake na tuhuma aliyobandikwa, na akampwekesha Mola wake.
Na miongoni mwa aya zinazoshuhudilia ukweli wao: ni yale waliyokuwa juu yake kati ya mwenendo mwema, na tabia zilizonyooka, na yale Allah aliwatendea wao na wafuasi wao ya ushindi na kuwapa mwisho mwema, na aliyowatendea waliowakadhibisha ya uangamizi na adhabu.
Na Allah amemkusanyia Nabii wetu Muhammad ﷺ aya nyingi na kubwa zaidi kuliko alizowapa manabii amani iwashukie, Amesema shaykhul Islam Ibnu Taymiyyah – Allah amrehemu- "Na miujiza yake ni zaidi ya alfu moja, na hakuna katika ulimwengu elimu iliyopatikana kwa habari mutawaatir([3]) isipokuwa elimu inayohusiana na miujiza na sheria za dini ya Mtume ﷺ iko wazi zaidi". Amesema Allah Aliyetakasika: ﴾ Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uwongofu na dini iliyo ya haki, ili aifanye kuwa juu ya dini zote, na Allah anatosha kuwa shahidi﴿»
Katika aya za unabii wake: bishara ya manabii waliokuwa kabla yake kuhusu kuja kwake, alisema Ibrahimu na Ismāīl amani iwe juu yao: "﴾Ewe Mola wetu, mtumilize katika umma huu mjumbe katika kizazi cha Ismā'īl awasomee aya zako na awafundishe Kitabu na Sunnah, na awasafishe na ushirikina na tabia mbaya" ﴿
Na alisema 'Ĩsã amani iwe juu yake: ﴾Na ni mwenye kutoa habari njema ya Mtume atayekuja baada yangu ambaye jina lake litakuwa Ahmad﴿, na alimteremkia Malaika katika udogo wake, akakipasua kifua chake na kuitoa sehemu ya shetani iliyokuwemo.
Na kabla ya hajatumilizwa, Allah alimuepusha kutokana na mambo ya ujaahiliya na uchafu, kwa hivyo hakuonekana uchi, wala mkono wake haukugusa sanamu, wala hakunywa pombe, au kumuuzia yeyote kitu haramu.
Na ulinzi wa mbingu kwa vimondo ulizidishwa ili kuhifadhi ujumbe wake, walisema majini: ﴾Na kwamba sisi, tulitaka kufika mbinguni, tukaipata imejazwa Malaika wengi wenye kuilinda na vimondo vya moto ambavyo wanarushiwa wenye kuikaribia ﴿.
Na miongoni mwa alama za unabii wake kuna zile zilizopatikana katika uhai wake na zikabakia hadi leo kama vile Qur'ani Tukufu, na elimu na Imani iliyobebwa na wafuasi wake.
Na miongoni mwa alama za unabii wake; yale aliyoelezea kati ya yale aliyooneshwa na Allah miongoni mwa matukio mengi yaliyopita na ghaibu zinazokuja, kwa maelezo ya kina, ambayo hawezi yeyote kuyajua isipokuwa kwa kufahamishwa na Allah mwenye enzi na utukufu, Amesema Aliyetakasika: ﴾Hizi ni katika habari za ghaibu tulizokufunulia, hukuwa ukizijua wewe wala watu wako kabla ya hapa﴿.
Na miongoni mwa yale yaliyopita aliyotusimulia habari zake: habari ya Adam kusujudiwa malaika, na kuhusu Iblisi na kiburi chake, na maelezo mengi ya kina na ajabu katika visa vya manabii, na yale waliyohitilafiana juu yake umma zilizotangulia na habari ya watu wa pango, na watu wa ndovu.
Na Allah aliwapa viumbe changamoto waje na Sura mfano wa Qur'ani; kisha akabainisha kuwa hawataweza hilo mpaka siku ya kiyama, hakuweza yeyote, Na akatueleza kuhusu makafiri- hali Mtume ﷺ ni mnyonge katika mji wa Makkah- ﴾Utashindwa mkusanyiko wa makafiri wa Makkah na watakimbia﴿, na ukadhihiri ukweli wa maneno hayo baada ya miaka mingi, akawaonesha waislamu sehemu watazofia mabwana wa Kikureshi kwenye uwanja wa vita kabla ya siku ya Badr, akasema: «hapa ndipo ataangamia fulani, alisema Anas – radhi za Allah zimshukie – : Na huku anawekelea -yani Mtume ﷺ mkono wake - juu ya ardhi hapa na hapa, basi hakufia yeyote miongoni mwao mbali na sehemu aliyowekelea Mtume ﷺ mkono wake» (imepokewa na Muslim), Na alipotoka kuelekea Khaybar alileta takbiri na kusema: «Khaybar imeharibika», Allah akampa ushindi juu ya watu wa Khaybar (imepokewa na Bukhari na Muslim).
Na alipowatuma Masahaba wake kwenda vita vya Mu-ta ili kupigana na Warumi, aliwapa watu habari za vifo vya mashahidi kati yao kabla ya kufikiwa na habari yao (imepokewa na Bukhari).
Na akabashiri kuwa Wafursi watawashinda Warumi katika uhai wake, na alipomjia mjumbe na barua kutoka kwa Kisra, alimwambia: «Hakika Mola amemwangamiza amemwangamiza bwanako usiku huu ». (Ahmad).
Na alipokuwa njiani kuelekea Tabuk alisema: «Utavuma upepo mkali juu yenu usiku huu, basi asisimame yeyote miongoni mwenu» (Bukhari na Muslim).
Pia alisimulia ukaribu wa kifo chake na kuungana na wema waliotangulia kati ya mitume na wafuasi wao katika pepo, akakaa juu ya mimbari na akasema: «mja aliulizwa na Allah achague baina ya starehe za dunia, na yale yaliyo kwake (yani kwa Allah), akachagua yaliyo kwa Allah! Abu Bakr -radhi za Allah zimshukie- akalia na kusema, tunawatoa baba zetu na mama zetu fidia kwa ajili yako! » (Bukhari na Muslim), baada ya kusema maneno haya, hakukaa siku nyingi hadi kuaga dunia, vilevile, alisema kuwa baada ya miaka mia moja hatabaki yeyote miongoni mwa maswahaba wake juu ya mgongo wa ardhi (Bukhari na Muslim), yote hayo yakawa kama alivyotabiria ﷺ.
Na akabashiria ufunguzi wa Baitil Maqdis, na kuwa baada yake kutazuka ugonjwa wa tauni utakaoangamiza idadi kubwa ya waislamu, na kwamba baada ya hapo mali yatakithiri asipatikane yoyote wa kupokezwa, ikawa kama alivyoeleza; ukapatikana ufunguzi wa Baitil Maqdis, na tauni ikazuka upande wa Sham, matukio haya mawili yalitukia katika uongozi wa Khalifah U'mar -radhi za Allah zimshukie -, kisha mali yakakithiri wakati wa uongozi wa U'thmãn bin A'ffãn -radhi za Allah zimshukie – ikawa hata akipewa mmoja wao dinari mia moja hachukui kwa kuwa amejitosheleza.
Na akatufahamisha kuwa waislamu wataishinda miji na kuitawala, na kwamba wakazi wa mji wa Madina watagura na kuielekea miji hio ili kupata starehe na upana wa riziki, na akasema: « Na madina ni bora kwao lau wangalijua» (Bukhari na Muslim), kama alivyobashiria kumalizika ufalme wa Kisra na Kaisari na kwamba hazina zao zitatumika kwenye njia ya Allah, vilevile alieleza kuwa umma wake utafunguliwa na kukunjuliwa dunia, waifanyie pupa kama walivyofanya waliokuwa kabla yao, na kwamba umma wake watajifananisha na umma waliopita na kufuata njia zao hata lau wataingia kwenye shimo la burukenge wataingia (Bukhari na Muslim).
Na akabainisha alama za kiyama zitakazotukia kabla ya kusimama kwake: miongoni mwa upungufu wa elimu, na wingi wa ujinga, na kutokea fitina, na wingi wa mauaji, na kushindana katika urefushaji wa mijengo; alisimama siku moja baina ya maswahaba wake akawafafanulia yale yatakayokuwa kabla ya Kiyama, Amesema Hudhaifa -radhi za Allah zimshukie- «Alisimama Mtume wa Allah -rehema na amani zimshukie- kisimamo, hakuacha chochote kitakachotukia wakati ule hadi siku ya kiyama isipokuwa alisimulia kukihusu, akahifadhi mwenye kuhifadhi, na akasahau mwenye kusahau» (Bukhari na Muslim).
Pia, akawahadithia Maswahaba wake aliyoyashuhudia na kuyaona mbinguni, - katika safari ya al-Israa wa al-Mi'raaj - Allah alipompeleka kwa roho yake na mwili wake kutoka Makkah hadi msikiti wa Aqsa ulioko Bayt al- Maqdis, kisha akampandisha juu mbinguni mpaka akafika kwenye Sidra al-Muntaha([4]), kisha akarejea Makkah usiku ule ule, akawafahamisha aliyoyaona ya Pepo na wakaazi wake na Moto na watu wake na sidra al-Muntaha, na sauti ya mwandiko wa kalamu za makadirio ya ulimwengu.
Vilevile, Allah alimpa nguvu kwa aya za kilimwengu zenye kuonekana kwenye viumbe kwa macho: akampasulia mwezi mpaka ukawa pande mbili, wakashuhudia watu Makkah na miji mingine.
Na alama za unabii wake zilionekana kwenye miili ya wanadamu: kwa mfano, katika hotuba ya hija ya kuaga, Allah aliyafungua maskizi ya watu mpaka wakamskia wote, idadi yao ilikuwa zaidi ya elfu mia moja (Abu Dawuud).
Alimuombea Anas -radhi za Allah ziwe naye- Allah ampe watoto wengi na mali mengi; ikawa hivyo na akashuhudia katika uhai wake janaza za watu zaidi ya mia moja na ishirini katika kizazi chake (Bukhari na Muslim).
Na akawaombea Abu Hurayra na mamake -radhi za Allah ziwe nao wote wawili- kwamba Allah awaruzuku mapenzi ya waumini, amesema Abu Hurayra: «Hakuumbwa mumini yeyote, akaskia kunihusu isipokuwa alinipenda hata kama hajaniona» (Muslim).
Na akamuombea U'rwah al-Baariqiy – radhi za Allah zimshukie- apate baraka katika ununuaji na uuzaji wake; akawa hata lau angeuza mchanga basi angepata faida (Bukhari).
Na ulipovunjika mguu wa Abdullahi bin A'tiik -radhi za Allah zimshukie-, Mtume ﷺ aliupangusa; ukapona (Bukhari).
Na aliyatemea mate macho ya Ali – radhi za Allah zimshukie- yalipokuwa yameugua; akapona kama vile hakuwa ameumwa kabla ya hapo (Bukhari na Muslim).
Vilivile, alama za unabii wake zilidhihiri kwenye wanyama-kaya (mifugo): Mtume ﷺ siku moja aliingia kwenye bustani ya baadhi ya Answaar akampata ngamia, naye ngamia akalia alipomuona Mtume wa Allah ﷺ, hapo akampapasa akanyamaza, kisha akamwambia mwenye ngamia: «Kwani Humuogopi Allah kwa huyu mnyama aliyokumilikisha Allah?! Hakika amenishtakia kuwa unamuweka na njaa na kumtaabisha» (imepokewa na Abu Dawuud).
Na alisema A'isha -radhi za Allah zimshukie-: « familia ya Mtume ﷺ ilikuwa na mnyama, kila akitoka Mtume ﷺ anacheza kwa wingi sana, lakini anapomhisi Mtume ﷺ ameingia, mnyama huyo anajilaza na kunyamaza kimya, wakati ule Mtume ﷺ atakuwa nyumbani; kwa kuogopea kumuudhi» (imepokewa na Ahmad).
Na miongoni mwa alama za unabii wake, ni uwezo aliopewa na Allah wa kukihirisha chakula na kinywaji; katika Al-Hudaiybiyah walikuwa pamoja naye maswahaba elfu moja na mia tano, Amesema Jaabir -radhi za Allah zimshukie-: « Mtume ﷺ aliweka mkono wake ndani ya chombo, maji yakabubujika kwa nguvu katikati ya vidole vyake kama chemchemi, tukayanywa na kuyatawadhia, akaulizwa: mlikuwa wangapi? Akasema: Lau tungalikuwa elfu mia moja, basi maji hayo yangelitutosheleza, tulikuwa elfu na mia tano» (Bukhari).
Na katika vita vya Dhaat Al-Riqaa', aliyakusanya maji kidogo kwenye bakuli; maaskari wote wakajaza vyombo vyao maji hayo.
Na chakula kilipopungua katika vita vya Khaybar, Mtume ﷺ akawaamuru maswahaba wakusanye chakula chote walichokuwa nacho, akakiombea kipate baraka, wakala mpaka wanajeshi wote wakashiba, ilikuwa idadi yao elfu moja na mia tano.
Na katika vita vya Tabuk, Maswahaba waliokuwa idadi yao takriban elfu thelathini walipatwa na shida ya maji, Mtume ﷺ akatawadha katika moja ya chemchemi za mji wa Tabuk, maji mengi yakamiminika kwa nguvu wakayatumia wote (imepokewa na Muslim).
Na Samurah bin Jundub -radhi za Allah zimshukie- alisema: «Tulikuwa na Mtume ﷺ tukila katika chombo kimoja kikubwa, kuanzia asubuhi hadi usiku, wakisimama watu kumi wanakaa watu kumi, tukasema: "chakula kilikuwa kikiongezwa kutoka wapi?", akasema: Ni kitu gani kinachokustaajabisha? Kilikuwa kikitoka upande huu, na huku anaashiria mbinguni» (imepokewa na Tirmithiy).
Na katika alama za unabii wake ni kwamba Allah alimdhalilishia miti na mawe: Aliposhukia katika bonde yeye na maswahaba wake, aliikamata miti miwili nayo ikamuandama na kushikana juu yake kwa kutii amri yake (imepokewa na Muslim).
Na akiwa Makkah, majini walikusanyika kusikiliza kisomo chake cha Qur'ani, mti uliokua pambizoni mwake ukampa habari ya kuhudhuria kwao (Bukhari na Muslim).
Na alikuwa akiwahutubia watu akiwa juu ya gogo la mti kisha akatengenezewa mimbar, alipoanza kuitumia, gogo lile lilitoa sauti na kulia kilio cha mtoto, hadi pale alipowekelea Mtume ﷺ mkono wake; likanyamaza (imepokewa na Bukhari).
Na alisema Mtume ﷺ: «Hakika mimi najua jiwe Makkah liliokuwa likinisalimia kabla sijatumilizwa, Mimi hata sasa nalijua» (imepokewa na Muslim).
Na alipopanda juu ya mlima wa Uhud pamoja na kundi la Maswahaba wachache jabali liliwatetemesha, Mtume ﷺ aliligonga na kusema: «Tulia Uhud»; likathibiti (imepokewa na Bukhari).
Na katika alama za unabii wake ni kwamba, Allah alimtia nguvu kwa Malaika wake, jambo ambalo hakuwafanyia waliokuwa kabla yake; huko Makkah, Malaika wa majabali alimuomba ruhusa awafunike makafiri wa Makkah kwa al-akhshabain- nayo ni majabali mawili Makkah.
Ama kuhusiana na Hijra (kugura kutoka Makkah kuelekea Madina); Amesema Allah: ﴾Na yeye ni wa pili kati ya wawili (yeye na Abu Bakr al-swiddiiq- radhi za Allah zimshukie-) walipokuwa pangoni katika jabali la Thawr, Mtume akamwambia: "Usihuzunike kwa Yakini Allah yuko pamoja nasi", Allah akamteremshia utulivu wake, na akamnusuru kwa majeshi msiyoyaona﴿.
Na katika vita vya Badr; wabora wa Malaika -Jibriil na Mikaail- walishirikiana na Mtume ﷺ kuwapiga makafiri, pia alionekana Mtume ﷺ kwenye vita vya Uhud akiwa baina ya Malaika wawili waliokuwa wakipigana kwa ushujaa mwingi (Bukhari na Muslim), vilevile, Jibriil -amani imshukie- alitembea pamoja naye kutoka Al-Khandaq (mtaro uliokuwa ndani mji wa Madina) hadi Kijiji cha Bani Quraidhwa (imepokewa na Bukhari).
Na miongoni mwa alama za unabii wake ﷺ; ni kwamba Allah amemuhifadhi kutokana na shari za maadui wake, Amesema Allah Mtukufu:﴾Na Allah ni mwenye kukulinda na kukuokoa na maadui zako﴿, kwa hivyo hawakuweza kumuangamiza mpaka akanusirika juu yao pamoja na wingi wao na nguvu zao nyingi.
Na baadhi ya mayahudi walipomfanyia uchawi; Allah Mtukufu alimpa ushindi juu ya uchawi wao, akamjulisha kuwa amefanyiwa uchawi na akamwelekeza sehemu walipokuwa wameuficha na akaweza kuubatilisha, pia walimuekea sumu kwenye nyama ya mbuzi ili kumuua, Allah Mtukufu akamjuza hayo.
Na miongoni mwa alama za unabii wake ﷺ; tabia zake njema na maumbile yake yaliyokamilika.
Pamoja na kupata ushindi, na kutiiwa na viumbe, na kumtanguliza kwao kuliko nafsi zao na mali yao, Mtume ﷺ alifariki bila ya kuwacha dirham (fedha) wala diinaar (dhahabu), wala mbuzi wala ngamia, isipokuwa nyumbu yake na silaha yake na ngao yake aliyokuwa ameiweka rehani kwa myahudi kwa ajili ya deni la pishi (swaa') thelathini za ngano (aina ya nafaka) aliowanunulia familia yake.
Na baada ya hayo, Enyi Waislamu:
Atakayeyatafakari maisha ya Mtume ﷺ kuanzia kuzaliwa kwake hadi kufa kwake; atajua kwa yakini kuwa yeye ni Mtume wa Allah, alikuja na maneno ambayo, viumbe wote tangu wa mwanzo hadi wa mwisho wao hawajapata kuskia mfano wake, na alikuwa kila wakati anawaamuru na kuwalingania watu kumpwekesha Allah katika ibada, na kuwaelekeza kwenye kila la kheri, na kuwakataza kila lenye shari, na Allah alikuwa akimdhihirishia aya nyingi zenye maajabu.
Alikuja na dini kamili zaidi, iliyokusanya mazuri yaliyokuwa katika umma zilizopita, ukawa umma wake ndio umma mkamilifu zaidi katika kila jema, na hawakuyapata mema haya isipokuwa kupitia kwake na kusoma kutoka kwake, naye ndiye aliyewaamrisha kuyatekeleza na kujipamba nayo, wakawa ndio wasomi wakubwa wa watu wa duniani na wenye kushikana na dini zaidi na waadilifu zaidi na wabora wao.
Najilinda kwa Allah kutokana na Shetani aliyefukuzwa kutoka kwa Rehema ya Allah,
﴾Sema, Ewe Mtume, "Bila shaka mimi ni binadamu kama nyinyi, ninaletewa wahyi kutoka kwa Mola wangu ya kwamba mola wenu ni Mola Mmoja tu. Basi yeyote anayetumaini kukutana na Mola wake na kupata malipo yake, naafanye matendo mema wala asimshirikishe yoyote katika ibada ya Mola wake"﴿
Allah atubarikie mimi na nyinyi katika Qur'ani Tukufu…
Hotuba Ya Pili
Sifa njema zote ni za Allah kwa ihsani yake, na Shukrani ni zake kwa taufiki yake na vipaji vyake, Nashuhudia kwamba hapana apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah peke yake hana mshirika kwa kuitukuza shani yake, Na nashuhudia kwamba Muhammad ni mja wake na Mtume wake, rehema za Allah zimshukie yeye na familia yake na maswahaba wake na awape salamu nyingi.
Enyi Waislamu:
Kuzitafakari alama za unabii wa Muhammad ﷺ na dalili za ukweli wake inazidisha katika imani, na kusoma kwa wingi mazuri yake yenye kuvutia na sheria yake tukufu ni sababu ya kupata daraja za juu, na hatuwezi kumjua Allah isipokuwa kupitia njia yake ﷺ.
Na anayetaka kujua ukweli wa ujumbe wake na uwazi wa hoja zake, basi aisome Qur'ani Tukufu.
Na walipokuwa viumbe wahitajia zaidi kumsadikisha Mtume kuliko kuhitajia kwao vitu vyote; Allah alirahisisha alama ambazo kwazo unajulikana ukweli wa Manabii, na akazijaalia kuwa nyingi na wazi na zenye kushinda, kiasi ya kwamba hakatai kuamini isipokuwa mjeuri, wala haingiwi na shaka kuhusu ukweli wao isipokuwa mwenye kiburi.
Na kwa kweli, kheri yote iko katika kusimama imara kwenye kusadikisha unabii wa Muhammad ﷺ na kumtii.
Kisha mjue kuwa Allah amewaamrisheni kumuombea Nabii wake rehema na amani …
([1]) Hotuba hii ilitolewa siku ya Ijumaa, Tarehe: 21/05/1443H, katika Al-Masjid Annabawwiy, mji wa Madina, Saudi Arabia.
(Dalaail annubuwwah: ni dalili na hoja ambazo kwazo mwanadamu anajua kuwa manabii wametimilizwa na Allah, na kwamba ni wakweli katika yale waliyofikisha).
([2]) (Fitra: ni hali ambayo Allah Mtukufu amewaumbia waja wake ya kumkubali na kumjua na kumpwekesha na kumwabudu).
([3]) (habari zinazopokewa na kupokezanwa na idadi kubwa ya watu katika kila zama)